Marekani imetoa onyo kali kwa washirika wake pamoja na China, ikiwataka kuunga mkono kampeni mpya ya kiuchumi inayolenga “kuangusha” serikali ya Iran, la sivyo wakabiliane na matokeo.
Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema nchi nyingine zinapaswa kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na Marekani au zikabiliwe na matokeo yake.
“Hii itakuwa operesheni kubwa zaidi ya kiuchumi iliyowahi kuratibiwa katika historia ya dunia. Na tunawaambia: mko pamoja nasi au mko dhidi yetu,” Waziri wa Marekani, Bessent aliliambia Shirika la Habai la CNBC siku ya Alhamisi, akieleza ujumbe anaowafikishia washirika wa Marekani.
Alipoulizwa iwapo Marekani itaishinikiza China, Bessent alisema, “Mazungumzo mengi ni bora yafanyike kwa faragha,” lakini akaongeza kuwa China inapaswa “kuunga mkono mpango huo.”
Bessent amewataka pia nchi nyingine duniani kufanya uamuzi wa kuunga mkono hatua za Marekani au kukabiliana na matokeo.
“Kwa hiyo, ni wakati wa washirika wetu na dunia nzima kufanya uamuzi, na tutaangusha uchumi wa utawala huu wa mauaji, jambo ambalo litapunguza uwezo wao wa kutumia washirika wao wa kijeshi na kisiasa kueneza ushawishi wao,” alisema.
Hapo awali, China ilipinga kampeni ya Rais Donald Trump ya kiuchumi dhidi ya Iran, ikisisitiza kwamba mzozo huo unapaswa kumalizwa kupitia diplomasia.
“Uwekaji wa vikwazo na shinikizo havisaidii kutatua suala hili,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, aliwaambia waandishi wa habari mjini Beijing.
“China inazitaka pande husika kuchukua hatua za kuwajibika na kutatua masuala hayo kupitia njia za kidiplomasia na kisiasa,” alisema Lin.
Washington imeweka mfululizo wa vikwazo vipya vya kiuchumi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwishoni mwa Februari. Hata hivyo, serikali ya Iran imeendelea kuhimili shinikizo hilo na kubaki madarakani.
Bessent, hata hivyo, anasisitiza kuwa awamu hii mpya ya vikwazo itafanikiwa na kwamba “tutaangusha utawala huu.”
Alisema pia kuwa shinikizo jipya la kiuchumi huenda likamaanisha kwamba, kwa sasa, hakutakuwa na ongezeko kubwa la operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran.
“Ikiwa tunatumia kiwango cha juu kabisa cha shinikizo la kiuchumi, basi hiyo ina maana kwamba kuna uwezekano mkubwa hakutakuwa na kuanza tena kwa operesheni kubwa za kijeshi. Lakini ninasisitiza kwamba hilo ni kwa sasa,” alisema.
Bessent alisema atafanya mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu ili kueleza kwa undani hatua zitakazohusika katika kampeni hiyo mpya ya shinikizo la kiuchumi.















