Shirika la Afya Duniani (WHO) lmesema kuwa bado kuna matumaini ya kudhibiti mlipuko wa Ebola ambao kwa sasa unaenea kwa kasi zaidi kuliko juhudi za kuudhibiti na ambao umekuwa mlipuko wa pili kwa ukali zaidi kuwahi kurekodiwa.
Shirika hilo la afya duniani lilisema mapema mwezi huu kuwa inawezekana kuzuia kuenea kwa Ebola ndani ya kipindi cha miezi mitatu, lakini tangu wakati huo kumekuwa na dalili za hali kuwa mbaya zaidi, huku mlipuko huo ukifika katika jimbo la sita.
“Kuhusu mpango wa miezi mitatu ijayo, ndiyo, iwapo rasilimali zinazohitajika zipo, nadhani inawezekana kufanya hivyo,” Thierno Balde, meneja wa WHO anayesimamia dharura hiyo, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kupitia mawasiliano ya video akitokea Bunia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
WHO inasema imefanikiwa kupata takriban asilimia 60 ya dola milioni 115 zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko huo wa Ebola.
Kuongezeka kwa juhudi za kudhibiti mlipuko
Hata hivyo, juhudi za kudhibiti mlipuko huo zinaongezwa nguvu na vitanda vingine 400 vimeongezwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, alisema Balde.
Kamati ya Dharura ya WHO inakutana Jumanne kujadili mlipuko huo, ambao shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuwa dharura ya kimataifa mnamo Mei 17.
Mlipuko wa Ebola nchini Congo, ambao unaenea kwa kasi, umesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,300 na kuwa mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Mlipuko huo unaoendelea katika mojawapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi nchini Congo ndio mlipuko wa Ebola unaoenea kwa kasi zaidi kuwahi kutokea, ukiwa na maambukizi 4,945 na vifo 2,325, kulingana na takwimu za serikali zilizotolewa usiku wa kuamkia Jumatatu.
Huu ni mlipuko wa 17 na mkubwa zaidi wa Ebola nchini Congo. Idadi ya vifo imezidi ile ya mlipuko wa mwaka 2018-2020, ambapo vifo 2,299 vilirekodiwa kati ya maambukizi 3,481.















