Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu imeahirishwa hadi Ijumaa ya Agosti 21 ambapo mahakama itaamua kama mwanasiasa huyo ana kesi ya kujibu au la.
Kesi hiyo, namba 19605/2025 ilianza kwa upande wa Jamhuri kufunga mashahidi wake 17 kati ya 30 ambao walitoa ushahidi wao.
Agosti 17, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru limesema linahitaji muda kuandaa uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za Lissu na upande wa jamhuri pamoja na kupitia ushahidi wa mashahidi 17 uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Awali katika hoja zake, Lissu aliieleza Mahakama kuwa hana kesi ya kujibu na kuiomba itamke kuwa hana hatia pamoja na kuamuru alipwe fidia.
Akirejea maamuzi mbalimbali ya mahakama, ikiwemo kesi ya Rambaklal Trambaklal Bhatt dhidi ya Jamhuri, Lissu amesema katika shtaka la uhaini, ni lazima kuwe na uthibitisho wa nia ya kufanya kitendo hicho, na nia hiyo inapaswa kuthibitishwa kupitia maandishi au matendo ya wazi.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalohusishwa na maneno aliyodaiwa kuyatamka kuhusu kusudio la kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.















