Rais Donald Trump wa Marekani amepuuzia hali za afya ya wanajeshi wa nchi hiyo waliopo ndani ya manowari ya kivita inayoendesha mashambulizi dhidi ya Iran.
Alipoulizwa siku ya ijumaa, iwapo wanafamilia wa askari walikuwa na wasiwasi wa afya ya ndugu zao, Trump alisema:
“La hasha, sidhani.”
Katika hatua nyingine, Trump alikana madai kuwa manowari hiyo ya Abraham Lincoln, ambayo ipo majini kwa miezi tisa sasa, ilikuwa imekaa baharini kwa muda mrefu.
Trump alisisitiza kuwa, si kweli kuwa chombo hicho kipo majini kwa muda mrefu, akiongeza kuwa siku chache zijazo, manowari nyingine itawasili kwa shughuli kama hiyo katika eneo hilo.
“Manowari ya Abraham Lincoln inaendelea na shughuli zake, na siku chache zijazo, kutakuwa na meli kama hiyo hiyo kwa shughuli za kijeshi,” alifafanua Trump.
Vyombo vya habari vya Marekani, wakiwemo wataalamu wa masuala ya kivita, wamewanukuu ndugu za wanajeshi hao, wakisema kuwa hali za afya za wapiganaji hao zinazidi kudhoofika.
Hali kadhalika, kumekuwepo na fununu za baadhi ya askari kutaka kujiua wakiwa ndani ya meli hiyo, huku wanasiasa wa upande wa Democratic wakitaka uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.















