Idadi ya simba nchini Tanzania, imefikia 17,200, kulingana na utafiti uliotolewa Juni 17, 2026.
Matokeo ya sensa iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), yameiweka Tanzania katika nafasi ya kwanza barani Afrika, kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao, maarufu kama ‘Mfalme wa Nyika’.
Wakati Tanzania ikiongoza kwa kuwa na simba 17,200, Afrika Kusini ipo katika nafasi ya pili ikiwa na simba 3,284, Botswana 3,064, Kenya 2,515 na Zambia 2,349.
Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake katika uhifadhi wa wanyamapori, baada ya idadi ya nyati nchini humo, kufikia 328,000, na kushika nafasi ya kwanza barani Afrika.
Nchi hiyo inafuatiwa na Afrika Kusini yenye nyati 46,000, Msumbiji 45,000, Kenya 42,000 na Zambia yenye nyati 41,000.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matokeo ya sensa hiyo jijini Arusha, Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Jublet Mjingo amesema kuwa, sensa yam waka 2024/2025 imefanyika miaka 10 baada ya ile ya mwaka 2014/2015 na kwa mara ya kwanza, imehusisha mifumo yote ya ikolojia nchini humo.















