Gari moja limegongana na ndovu katika mbuga ya wanyama nchini Uganda, na kusababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi wengine wanne, polisi wanasema.
Ajali hiyo ilitokea siku ya Jumapili katika barabara ndani ya Mbuga ya Taifa ya Murchison, polisi waliseama katika taarifa Jumatatu.
Gari hilo lilikuwa limewabeba wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Uganda waliokuwa wamesafiri kutoka mji wa kaskazini kwa Uganda hadi mji mkuu wa Kampala.
Baada ya kumgonga mnyama huyo, dereva “alishindwa kudhibiti gari”, taarifa ya polisi ilisema. “Madereva wanatakiwa kuwa makini sana wakati wanapoendesha kupitia mbuga za taifa na maeneo yenye wanyamapori.”
Video kutoka eneo hilo inaonesha watu waliokuwa ndani ya gari wakiomba msaada huku ndovu ambaye aliyekuwa amejeruhiwa akijikokota kusimama karibu na msitu. Haikufahamika kama ndovu alinusurika katika ajali hiyo.
Pamoja na kuwa matukio haya ni nadra, yanadhihirisha kile wanamazingira wanakitaja kuwa mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori ambao unaweza kuibuka katika maeneo ya hifadhi ambayo watu wanatumia.
















