Sudan Kusini yaamuru kuhamishwa kwa maafisa wa UN katika kaunti tatu kabla ya opresheni ya kijeshi

Serikali ya Sudan Kusini imesema operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la “Operation Enduring Peace” iko karibu kuanza.

Newstimehub

Newstimehub

26 Januari, 2026

f763c1f208bc0acb688774edd805db778cc940621050f83f1db11342a4107d5c

Jeshi la Sudan Kusini limewaamuru raia wote pamoja na wafanyakazi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kuondoka katika kaunti tatu za Jimbo la Jonglei kabla ya kuanza kwa operesheni dhidi ya vikosi vya upinzani.

Mapigano ambayo Umoja wa Mataifa unasema hayajawahi kufikia kiwango kama hiki tangu mwaka 2017 yameikumba Sudan Kusini kwa miezi kadhaa. Nchi ambayo ni taifa changa zaidi barani Afrika.

Baadhi ya mapigano makali zaidi yamekuwa yakitokea Jonglei, eneo lililoko mashariki mwa nchi karibu na mpaka wa Ethiopia, ambako Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) linajaribu kuzuia mashambulizi ya wapiganaji washirika wa Jeshi la Ukombozi wa Wananchi wa Sudan – wa Upinzani (SPLA-IO).

Kwa mujibu wa taarifa ya uhamishaji iliyotolewa siku ya Jumapili, SSPDF ilisema kuwa operesheni hiyo iko “karibu kuanza”.

Uhamishaji ndani ya saa 48

Jeshi limesema raia wote wanaoishi katika kaunti za Nyirol, Uror na Akobo wameelekezwa kuondoka mara moja kwa usalama wao na kuelekea maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Wafanyakazi wote wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) pamoja na wale wa mashirika yasiyo ya kiserikali pia wameamrishwa kuondoka katika kaunti hizo tatu ndani ya saa 48.

Msemaji wa UNMISS aliambia shirika la habari la Reuters kuwa walinda amani wa UN waliopo Akobo bado wapo na wanaendelea kutekeleza jukumu lao la kupunguza mvutano na kuzuia mapigano. Hata hivyo, hakusema kama wafanyakazi wa UN bado wapo katika kaunti nyingine.

Wiki iliyopita, SPLA-IO iliwaagiza wapiganaji wake kuelekea mji mkuu wa nchi, Juba, jambo lililoashiria ongezeko kubwa la mzozo.

Mapigano makali

Mapema mwezi huu, vikosi vya SPLA-IO viliteka mji wa Pajut kaskazini mwa Jonglei baada ya mapigano makali. Kutekwa kwa mji huo kulionekana kuhatarisha usalama wa mji mkuu wa jimbo hilo, Bor.

Katika taarifa ya Jumapili, UNMISS ilisema watu 180,000 tayari wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo huo, na ikawataka viongozi wa Sudan Kusini “kuweka maslahi ya wananchi wao mbele kwa kusitisha mapigano”.

Shirika la madaktari la Médecins Sans Frontières (MSF) lilisema pia siku ya Jumapili kuwa limewaondoa wafanyakazi wake muhimu kutoka kaunti ya Akobo baada ya kupokea maelekezo wazi kutoka kwa mamlaka husika na kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama.

Vikosi vya SPLA-IO vinavyoongozwa na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, vilipigana na jeshi la serikali katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2013 na 2018. Vita hivyo, vilivyopiganwa kwa misingi ya kikabila, viliua takriban watu 400,000.