Shambulio lililofanywa na kundi la wanamgambo limewaua watu wasiopungua tisa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyanzo vya ndani vilisema Jumapili.
Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, kundi la Allied Democratic Forces (ADF) lilifanya mashambulizi dhidi ya raia katika mji wa Oicha, likipora maduka na kuchoma moto nyumba, kulingana na taarifa zilizokusanywa na shirika la habari la AFP eneo hilo.
Wakati wa “uvamizi huu, adui wa ADF aliwaua raia wanane na afisa mmoja wa polisi,” alisema Isaac Kavalami, rais wa kikundi cha kiraia cha eneo hilo, alipoongea na AFP.
Jumapili, mwandishi wa AFP aliona miili tisa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali Kuu ya Oicha, baadhi ikiwa na majeraha ya visu.