Wanajeshi wawili wa Somalia waliohukumiwa kifo kwa kula njama na kundi la kigaidi la Al Shabab kumuua kamanda walitekelezwa hukumu yao Jumatatu, maafisa wa mahakama ya kijeshi walisema.
Mahakama ya kijeshi katika mji mkuu Mogadishu iliwahukumu wanajeshi hao wawili kifo mnamo Agosti, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kamanda wa kikosi chao mnamo Julai.
Mmoja aligundulika kuwa alipokea kifaa cha mlipuko, huku wa pili akiweka kifaa hicho chini ya kitanda cha kamanda wao, kabla ya kulipuliwa kwa njia ya mbali.
“Walitekelezwa leo kwa kuhusika kwao katika mauaji ya Kamanda Aided Mohamed Ali,” alisema mwendesha mashtaka Hassan Siyad Mohamed.