Marekani imetangaza kusitisha maombi yote ya viza ya kawaida kwa raia wa Zimbabwe, ikiwa ni kikwazo cha hivi punde zaidi kwa wasafiri kutoka Afrika.
Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Alhamisi kwamba Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe utasitisha huduma zote za kawaida za viza kuanzia Ijumaa “huku tukishughulikia masuala hayo na Serikali ya Zimbabwe”.
Hili limekuja siku chache baada ya Marekani kuzindua mradi wa majaribio unaowataka raia wa nchi nyingine mbili za Afrika, Malawi na Zambia, kulipa dhamana ya hadi $15,000 kwa viza ya utalii au biashara.
Dhamana itaondolewa ikiwa muombaji atasalia Marekani baada ya muda wa viza yake kuisha.
Ubalozi huo ulielezea hatua hiyo kuhusu Zimbabwe kuwa ya muda na ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Trump za “kuzuia muda wa viza kuzidishwa na matumizi mabaya.”
Viza nyingi za kidiplomasia na zile zilizo rasmi hazitoathiriwa, Marekani ilisema.
Vikwazo vya kusafiri
Marekani imetekeleza vikwazo vipya vya usafiri kwa raia kutoka nchi kadhaa za Afrika chini ya sera pana za uhamiaji za Rais Donald Trump, huku ikizishinikiza nchi za Kiafrika kuwakubali watu waliofukuzwa kutoka Marekani ambao si raia wao.