Serikali ya Kenya imewarejesha nyumbani Wakenya 119 waliokuwa wamehadaiwa kwa ahadi za uongo za kazi, lakini baadaye wakalazimishwa kufanya shughuli za utapeli mtandaoni katika baadhi ya nchi za Asia ya Kusini-Mashariki.
Hata hivyo, mamia ya Wakenya wengine bado wapo nchini Myanmar, Thailand na Cambodia.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema kuwa kurejeshwa huko kulifuatia operesheni za hivi karibuni zilizofanywa kwa kushirikiana na mamlaka za Myanmar , zilizolenga makundi ya utapeli yaliyokuwa yakifanya kazi karibu na mpaka wa Thailand katika Jimbo la Karen.
Awali, jumla ya watu 126 walipangwa kurejeshwa nchini, lakini saba walilazimika kuahirisha safari zao dakika za mwisho. Wizara hiyo ilieleza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha Wakenya waliobaki wanarejeshwa salama, licha ya hali ngumu ya kiusalama na kisiasa katika eneo hilo.
Wizara hiyo ilifafanua kuwa mitandao ya kihalifu imekuwa ikiendesha vituo vya utapeli na kuajiri wafanyakazi kutoka mataifa mbalimbali duniani, wakiwemo Wakenya, mara nyingi kupitia matangazo ya kazi ya uongo.
Kwa sasa, Wakenya 198 wanasubiri kurejeshwa nyumbani. Kati yao, 66 wanazuiliwa katika Kituo cha Uhamiaji cha Thailand, huku 129 wakipewa hifadhi katika makazi ya muda nchini Myanmar.









