Serikali imezindua mradi mpya wa thamani ya shilingi bilioni 21.5 sawa na dola milioni 165.5 kwa ajili ya kurejesha na kusimamia kwa njia endelevu msitu wa Mau.
Mradi huu unajulikana kama Integrated Conservation and Livelihood Improvement Programme (MCF-ICLIP), unalenga kuboresha mifumo ya ikolojia, kuinua maisha ya jamii na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika eneo la Mau.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Festus Ng’eno, ambaye pia ndiye mlezi wa mpango huu, alisema kwamba Mau ni hazina kubwa kitaifa na kikanda.
“Thamani ya huduma na rasilimali za ikolojia zinazotolewa na msitu huu inakadiriwa kufikia shilingi bilioni 197. Msitu huu unasaidia jamii zinazouzunguka na pia kuisdia mifumo ya ikolojia mashuhuri kama vile Maasai Mara na Serengeti,” alisema Dkt. Ng’eno.
Msitu huu una ukubwa wa jumla ya ekari 403,000 na unajumuisha vitalu vya misitu 22. Ni msitu mkubwa zaidi unaopatikana kwenye mlima Afrika Mashariki, wenye bioanuwai ya kipekee duniani.