Jamii forums yafungiwa kwa siku 90 kwa ‘kudhalilisha serikali na Rais’ wa Tanzania

Aidha TCRA imeongeza kuwa maudhui hayo yanakinzana na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania, hivyo kuhatarisha mshikamano wa kitaifa, amani na taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Newstimehub

Newstimehub

6 Septemba, 2025

0f10c4a373cfa48e9d861a0e2745174f6b545606e081b59443f0046ab2b9ba76

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA amesitisha kwa muda wa siku 90, leseni ya huduma za maudhui mtandaoni iliyotolewa kwa kampuni ya Vapper Tech Limited, wamiliki wa jukwaa la Jamii Forums.

Jamii Forums inashutumiwa kuwa, kupitia mitandao yake imechapisha maudhui ya kupotosha umma, kukashifu na kudhalilisha Serikali pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika notisi iliyochapisha kwenye mtandao wake wa X, TCRA ilisema kuwa taarifa hizo inazodai kuwa potofu zilichapishwa mnamo Septemba 04, 2025 na kubainisha kwamba yamekiuka Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025.

“TCRA inapenda kuufahamisha umma kuwa, pamoja na kukiuka kanuni, maudhui hayo yanakinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania, jambo linaloweza kuathiri umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, na pia kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” —imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.