Macho na masikio ya Watanzania wote kwa sasa, yapo katika timu ya taifa ya nchi hiyo, maarufu kama ‘Taifa Stars’, itakapokuwa inasaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya CHAN 2024.
Kikosi cha Tanzania, kinachoongozwa na Hemed Suleiman Ali, maarufu kama kama ‘Morocco’, kitashuka kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kujaribu kuwapa furaha Watanzania, wanaposaka nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani.
‘Taifa Stars’, ambayo ilimaliza kundi B ikiwa na alama 10, na kushika nafasi ya kwanza, imekuwa na matokeo mabaya dhidi ya Morocco kwenye michuano ya kimataifa.

Katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, mchezo uliofanyika Machi 26, 2025, Tanzania ilikubali kufungwa mabao 2-0 na Morocco, iliyokuwa na akina Brahim Diaz wa Real Madrid na Achraf Hakimi wa PSG.