Afrika Kusini: Serikali yaanzisha upya uchunguzi wa kifo cha Albert Luthuli

Luthuli atakumbukwa kwa kukiongoza chama tawala cha ANC cha nchi hiyo kumaliza utawala wa wazungu wachache mwaka 1994.

Newstimehub

Newstimehub

15 Aprili, 2025

luthuli

Waendesha mashitaka wa Afrika Kusini wamefungua upya jalada la chanzo cha kifo cha Albert Luthuli, ikiwa ni miaka 58 toka kutokea kifo cha shujaa huyo aliyepambana  na ubaguzi wa rangi na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel.

Hii ni baada ya serikali ya nchi hiyo kusema kuwa kifo cha mwanaharakati huyo kilitokana na kukanyagwa na treni.

Luthuli atakumbukwa kwa kukiongoza chama tawala cha ANC cha nchi hiyo kumaliza utawala wa wazungu wachache mwaka 1994.

Hatua hiyo pia inakuja wakati mamlaka za uendeshaji mashitaka za Afrika Kusini zikipitia upya kesi zinazohusiana na sera ya ubaguzi wa rangi.

Kesi nyingine ambayo itapitiwa upya ni pamoja na kifo cha mwanaharakati Griffiths Mxenge, aliyeuwawa karibu na jiji la Durban mwaka 1981, kwa kuchomwa na kisu mara 45 na kukatwa koromeo.

Wakizungumza siku ya Jumatatu, waendesha mashitaka hao walisema kuwa watawasilisha ushahidi mpya kuonesha nia ya “kuficha na kuwalinda” wauaji wa Luthuli.

Waendesha mashitaka hao wametilia shaka mwenendo wa shauri na kesi ya awali, wakisisitiza kuwa kulikuwa na njama iliyowahusisha polisi, wapasuaji na maofisa mahakama.

Kwa muda mrefu sasa, familia ya Luthuli imetaka kuwepo na uchunguzi huru, huku wakitilia shaka mchakato wa awali.

Kwa upande wake, mjukuu wa Luthuli, Sandile Luthuli, aliliambia Shirika la Habari la Afrika Kusini, ameridhishwa na hatua ya kufungua upya jalada hilo.