Uturuki kuendelea na mipango ya maendeleo licha ya changamoto za kiusalama katika ukanda: Erdogan

Rais amesema Uturuki imefanikiwa kupunguza athari za migogoro ya kimataifa kwa kupanua wigo wa vyanzo vya nishati, kubuni njia mbalimbali za usambazaji na kutumia aina tofauti za nishati.

Newstimehub

Newstimehub

9 Novemba, 2026

d04d992d d5b5 4ac4 8142 ba9316829024 1794246322042

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema nchi yake itaendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo bila kuyumbishwa na hali ya taharuki na ukosefu wa utulivu katika ukanda, huku akieleza hatua zilizopigwa katika kuongeza uzalishaji wa nishati na kuimarisha usalama wa nishati nchini humo.

Erdogan amesema Uturuki imefanikiwa kupunguza athari za migogoro ya kimataifa kwa kupanua wigo wa vyanzo vya nishati, kubuni njia mbalimbali za usambazaji na kutumia aina tofauti za nishati. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa pia na juhudi za kidiplomasia zinazolenga kulinda maslahi ya nchi katika sekta ya nishati.

Akizungumza Jumatatu, baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika Ikulu ya Rais jijini Ankara, Erdogan amesema changamoto za kiusalama zinazoikabili kanda hiyo hazitaizuia Uturuki kuendelea na safari yake ya maendeleo.

“Licha ya misukosuko inayoikumba kanda inayotuzunguka, tunaendelea kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa utulivu na matumaini, bila kusimama,” amesema.

Katika hatua nyingine, Erdogan ametangaza kugunduliwa kwa maeneo mengine mawili yenye akiba ya mafuta. Amesema uzalishaji wa mafuta katika eneo husika unatarajiwa kufikia zaidi ya mapipa 100,000 kwa siku katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2027, kupitia visima takribani 230.

Ameeleza kuwa uzalishaji huo unatarajiwa kuingizia uchumi wa Uturuki mapato ya takribani Dola bilioni 4.4 za Marekani kila mwaka.

Akizungumzia suala la usalama wa nishati, Erdogan amesema serikali imeweka mikakati ya kupanua wigo wa vyanzo vya nishati. Kwa mujibu wake, hatua hiyo imeisaidia nchi kukabiliana na athari za migogoro ya kimataifa na kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa nishati.

Aidha, akizungumzia mpango wa kuifanya Uturuki kuwa nchi isiyo na ugaidi, rais huyo amesema maeneo ya mijini ambayo kwa muda mrefu yamekabiliwa na changamoto za kuhama kwa wakazi na ukosefu wa usalama yatapata fursa mpya za ukuaji na maendeleo baada ya ugaidi kutokomezwa kikamilifu.

“Ugaidi utakapoondolewa kabisa, ndipo Uturuki itakapopiga hatua kubwa zaidi katika ukuaji wake wa kiuchumi,” amesema.

Erdogan amesisitiza kuwa mpango huo hauhusu masuala ya usalama pekee, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa. Amesema serikali yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kutimiza dira ya kuijenga Uturuki yenye nguvu na uwezo mkubwa.