Makundi saba yenye silaha nchini Ethiopia, yakiwemo yale mahasimu kwa muda mrefu yaliyopigana yakiwa pande pinzani katika vita vya 2020-2022, yanasema yameunda muungano dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.
Kuanzishwa kwa Muungano wa Vikosi vya Watu wa Ethiopia kumeyaleta pamoja makundi kutoka kanda ya kaskazini ya Tigray hadi ile ya kusini ya Somali. Wengine bado wanazozana na baadhi ya wanachama kuhusu maeneo na masuala mengine.
Wasemaji wa Abiy na serikali kuu bado hawajajibu lolote kuhusu hilo.
Mwezi uliopita, baada ya ripoti kuibuka kuhusu kuundwa kwa muungano wa makundi yenye silaha, mshauri wa Abiy alisema muungano wowote wa aina hiyo utasababisha vurugu.
Muungano huo mpya, uliotangazwa Jumapili jioni, unajumuisha TPLF na Amhara Fano National Movement.
Fano, muungano wa makundi yenye silaha kutoka kanda ya Amhara, ulikuwa unaunga mkono serikali kuu dhidi ya TPLF wakati wa vita vya Tigray 2020-2022, vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuchochea uhasama miongoni mwa makabila tofauti.
Fano ikaanza vita dhidi ya serikali katika mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu Amhara tangu 2023.
Majadiliano ya Kitaifa
Mengi ya makundi hayo yameshtumu serikali kwa kuwa na madaraka makubwa na kuyatelekeza majimbo. Serikali inasema imeanzisha majadiliano ya kitaifa yenye lengo la kutatua tofauti za kisiasa na mapigano ya ndani.
“Sisi, vikosi vya watu vyenye lengo la kuona watu wa Ethiopia wanaishi, tuna jukumu la kihistoria la kupindua utawala huu,” walisema katika taarifa iliyosomwa na kiongozi wa Fano Zemene Kassie na kuoneshwa kwenye televisheni ya Tigray.
Tangazo hilo la muungano, ambalo linajumuisha makundi kutoka kanda za Oromia, Afar na Benishangul-Gumuz, linafuatia mapigano kati ya vikosi vya serikali kuu na vile vya Tigray.















