Kenya yahodhi Mkutano kati ya Afrika na Ufaransa

Rais William Ruto wa Kenya amesema uamuzi wa kuandaa mkutano huo kwa mara ya kwanza katika nchi isiyozungumza Kifaransa, ni uthibitisho mkubwa wa kukua kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Newstimehub

Newstimehub

11 Mei, 2026

2026 05 10t140125z 475742406 rc2d6lawi8vq rtrmadp 3 france kenya state visit

Rais William Ruto wa Kenya mwishoni mwa juma alimkaribisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika Ikulu ya Nairobi, kabla ya Mkutano wa siku mbili wa Africa Forward Summit unaoanza leo jijini Nairobi.

Rais William Ruto amesema kuwa uamuzi wa kuandaa mkutano huo kwa mara ya kwanza katika nchi isiyozungumza Kifaransa, ni uthibitisho mkubwa wa uhusiano unaokua kati ya nchi hizo mbili.

Ziara ya Macron inajiri wakati Ufaransa ikijaribu kurekebisha sera yake ya Afrika kufuatia kujiondoa kijeshi kutoka mataifa ya Sahel na kugeukia washirika wasio wa Francophone kama Kenya, huku kukiwa na ongezeko la ushindani kutoka kwa mataifa yenye nguvu ya kimataifa kwa ajili ya ushawishi katika bara hilo.

Ziara hiyo inajiri huku wachambuzi wakihoji uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Kenya na Ufaransa tayari zimesaini mikataba ya uboreshaji wa Kituo cha Reli ya Embakasi, mauzo ya chai ya zambarau ya daraja la juu nchini Kenya, matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, na maendeleo ya mradi wa Bwawa la Masinga.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, uzalishaji endelevu wa mafuta ya anga, mabadiliko ya kidijitali, upanuzi wa uwezo wa kuhifadhi makontena bandarini, na uchumi wa buluu na uvuvi.

Rais Ruto aliongeza kusema kuwa Kenya na Ufaransa zimedumisha uhusiano thabiti wa kidiplomasia tangu 1963.

Viongozi wengine waliowasili kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, antonio Gutteres, Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu, Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Jenerali Brice Oligui Nguema ambaye ni Rais wa Gabon.

Pia Rais Julius Maada Bio wa Sierra Leone, Nyuma Boakai wa Liberia na Alassane Ouattara wa Ivory Coast wamehudhuria.

Aziz Akhannouch, Mkuu wa Serikali ya Ufalme wa Morocco na Waziri Mkuu Navinchandra Ramgoolam wa Mauritius pia wako Nairobi katika mkutano huo wa siku mbili. Kwa upande wake, Tanzania inawakilishwa na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.