Waasi wa ADF waliokuwa wamejihami kwa mapanga na majembe wamewaua angalau raia 52 katika maeneo ya Beni na Lubero mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika siku za hivi karibuni, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa eneo hilo wamesema.
Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) walikuwa wakilipa kisasi dhidi ya raia baada ya kushindwa na vikosi vya Congo, alisema Luteni Elongo Kyondwa Marx, msemaji wa jeshi la eneo hilo.
“Walipofika, waliamsha wakazi kwanza, wakawakusanya mahali pamoja, wakawafunga kwa kamba, kisha wakaanza kuwachinja,” alisema Macaire Sivikunula, mkuu wa sekta ya Bapere huko Lubero, alipoongea na Reuters mwishoni mwa wiki.
Takriban raia 30 waliuawa katika kijiji cha Melia pekee, alisema Alain Kiwewe, msimamizi wa kijeshi wa eneo la Lubero, alipoongea na Reuters.
Wanawake na watoto miongoni mwa waathiriwa
“Miongoni mwa waathiriwa walikuwemo watoto na wanawake, huku nyumba kadhaa zikichomwa moto,” alisema.