Chama Cha Demokrasia na Maendeleo cha nchini Tanzania (CHADEMA) kimeiandikia barua ya malalamiko, kamati ya maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ikiilalamikia klabu ya soka ya Young Africans, kwa madai ya kujihusisha na siasa nchini humo.
Katika barua yake ya Agosti 15, 2025, chama hicho cha upinzani kimeitaka FIFA kuichukulia hatua klabu ya Young Africans kwa madai ya ukiukwaji wa kanuni za michezo ambazo zinaweka msisitizo kwenye ‘uhuru’ wa kutokuegemea upande wowote.
Katika harambee iliyofanyika Agosti 12 jijini Dar es Salaam, klabu ya Young Africans ilitoa kiasi cha milioni 100 kuisadia CCM katika kampeni zake, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Hali kadhalika, katika harambee hiyo hiyo, mdhamini na mfadhili wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed alitoa shilingi Bilioni 10 kama mchango wake kusaidia kampeni za Wagombea wa Urais wa chama hicho.