Wahamiaji 68 kutoka Afrika wafariki katika pwani ya Yemen baada ya boti kupinduka

Takriban wahamiaji 68 kutoka Afriki wamefariki na wengine 74 hawajulikani walipo baada ya boti kupinduka katika pwani ya Yemen, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji.

Newstimehub

Newstimehub

4 Agosti, 2025

82c3196f66b02716adc06d46adbf136809a9f46de871c1a7d236c48be45dd4f9

Mkasa huo ni muendelezo wa msururu wa ajali za meli kutoka Yemen na kuua mamia ya wahamiaji wa kutoka Afrika wanaokimbia migogoro na umaskini kwa matumaini ya kufika katika nchi tajiri za Ghuba ya Kiarabu.

Boti hiyo, ikiwa na wahamiaji 154 wa Ethiopia, ilizama katika Ghuba ya Aden karibu na mkoa wa kusini mwa Yemen wa Abyan mapema Jumapili, Abdusattor Esoev, mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Yemen aliambia shirika la habari la The Associated Press.

Alisema miili ya wahamiaji 54 ilipatikana ufukweni katika wilaya ya Khanfar, na wengine 14 walipatikana wamekufa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali huko Zinjibar, mji mkuu wa mkoa wa Abyan kwenye pwani ya kusini ya Yemen.

Ni wahamiaji 12 pekee walionusurika kwenye ajali ya boti, na wengine wote walipotea na kudhaniwa kuwa wamekufa, Esoev alisema.

Katika taarifa, idara ya usalama ya Abyan ilielezea ya kwamba operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea.

Licha ya zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, Yemen ni njia kuu ya wahamiaji kutoka Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wanaojaribu kufika nchi za Ghuba ya Kiarabu kufanya kazi.

Wahamiaji huchukuliwa na wasafirishaji haramu kwenye boti ambazo mara nyingi ni hatari, zilizojaa kupita kiasi katika Bahari Nyekundu au Ghuba ya Aden.