Serikali ya DRC, M23 wakubali kufanya mazungumzo

Taarifa iliyotolewa katika mazungumzo imethibitisha kwamba pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mapigano mara moja.

Newstimehub

Newstimehub

24 Aprili, 2025

1743773166939 nhqpo gettyimages 2200503809 20 1 scaled

Kundi la Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), vuguvugu la waasi ambalo linajumuisha waasi wa M23, lilikubali kufanya kazi ya kufikia mapatano na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati wa mazungumzo ya hivi karibuni yaliyosimamiwa na Qatar huko Doha.

Hii ni kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano.

Uamuzi huo ulifikiwa katika hali ya maelewano na dhamira ya pamoja ya kusuluhisha mzozo wa mashariki mwa DRC kwa njia za amani.

“Baada ya majadiliano ya wazi na yenye kujenga” wawakilishi wa serikali na AFC/M23 “walikubaliana kufanya kazi ili kuhitimisha makubaliano ambayo yangechangia ufanisi wa usitishaji wa mapigano,” taarifa hiyo ilisema.

Kulingana na taarifa hiyo, pande zote mbili zilithibitisha kujitolea kwao kusitisha mara moja uhasama ambao ungefungua njia ya mazungumzo yenye kujenga na kurudisha amani ya kudumu nchini DRC na kanda.

Kundi la M23, ambalo ni kitovu cha mzozo mashariki mwa DRC, limezidisha mashambulizi yake tangu Disemba 2024, na kuteka miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu.

Maamuzi ya awali

Mnamo mwezi Machi, wanajeshi wa DRC na waasi walitangaza uamuzi wa kusitisha mapigano ulioitishwa na Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wakati wa mazungumzo yaliyopatanishwa na Emir wa Qatar mnamo Machi 18 huko Doha.

Lakini hii imekiukwa tangu wakati huo, huku mapigano yakiripotiwa katika maeneo kadhaa katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi nyingine zinaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23.

Rwanda, hata hivyo, inakanusha madai hayo.

Kuongezeka kwa mapigano ya hivi majuzi kumewalazimu raia wa DRC kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani kutafuta usalama.

Takriban watu 120,000 wamewasili nchini Burundi, Tanzania na Uganda hadi sasa, kulingana na UN.